Diwani ya kwanza ya TUEHU

Diwani ya Tunzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein ni matunda la shindano la kwanza la Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein lililofanyika mwaka 2014. Tuzo hii ilianzishwa na Hayati Bwana Gerald Belkin, muongoza filamu aliyekuja Tanzania kutengeneza filamu juu ya maisha na changamoto za ujenzi wa ujamaa vijijini miaka ya 1960 na 1970. Belkin alifanya kazi bega kwa bega a Profesa Ebrahim Husein, mwanazuoni maarufu na mwandishi wa Tamthliya na mashairi. Kupitia kwa Ebrahim Hussein, Belkin alivutiwa sana na utamaduni wa Kiswahili hususani ushairi. Katika wasia wake aliacha fungu la fedha ili zitumike kuwashindanisha washairi wa Tanzania na Tuzo itolewe kwa washidi watatu wa kwanza. Belkin alianzisha Tuzo hii ili kuuenzi mchango wa rafiki yake, Ebrahim Hussein katika kuijenga fasihi ya Kiswahili.

Kwa upande wake Profesa Ebrahim Hussein metoa mchango mkubwa katika utunzi, uchambuzi na falsafa ya fasihi hususani ya Kiswahili. Vitabu vyake mfano: Kinjeketile, Mashetani, Wkati Ukuta, na Kwenye Ukingo wa Thim vimebeba fikra nzito juu ya mogogoro ya kiuchumi-Kisiasa, Kijamii na kiutamaduni inayotokana na mabadiliko ya kihistoria nchini Tanzania na Barani Africa kabla na baada ya Uhuru. Lakini jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba kazi hizo bora hivi leo hazipatikani kwa wingi wala kufundishwa shuleni nchini Tanzania. Diwani hii ni chapisho la kwanza la Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein.

Bodi ya uratibu ya shindano hili iliazimia kwamba tungo bora za shindano za kila mwaka ziwe kinachapishwa katika Diwani maalum ili kiweze kusomwa na watu wengi zaidi. Hivyo Diwani hii ya kwanza ina mashairi teule ya washindi na washiriki wengine wa shindano, pamoja na tafsiri za Kiingereza za mashairi ya washindi watatu wa kwanza. Ni matarajio yetu kuwa Diwani nyingine zitakuwa zikichapishwa kadiri shindano linavyoendelea kufanyika. Mashairi yaliyomo kwenye Diwani hii yametungwa na washairi mchangaiko – vijana, watu wazima, wazee, wanawake, wanaume, wafanyakazi, wasomi, wakulima n.k. Kwa pamoja mashairi hayo yanasawiri hali halisi ya maisha ya Watanzania na Waafrika kwa ujumla wao katika kipindi hiki na kubainisha mitazamo anuai ya wananchi wa kawaida kuhusu hali hiyo na kuhusu mustakabali wa nchi yao na bara lao la Afrika. Diwani hii inafaa kusomwa na watu wote wanaojali hali na hatma ya Mwafrika.

TABARUKU.

Uhai wa Tunzo ya Usahiri ya Ebrahim Hussein ulitegemea sana jinsi wazo la kuianzisha lilivyopokelewa. Kamati ya Uendeshaji wa Tunzo ilipoundwa tu, iliingia kazini, shindano likatangazwa, washindani wakajitokeza, jopo la majaji likafanya kazi yake na washindi wakapatikana na kutunukiwa Tunzo mbele ya hadhara. Kazi hii ilifanywa chini ya uongozi mahiri wa mwenyekiti wa kwanza, Bw. Ibrahim Seushi, ambaye sasa ni marehemu. Kwa kuuenzi mchango wake, tunaitabaruku Diwani hii kwa heshima yake.